KIBIRITI ni kitu gani? kama kinavyozungumziwa kwenye maandiko?

john7

Lister


Kibiriti tofauti na kinavyojulikana leo kwamba, ni kipande kidogo cha boksi kilichojaa chiti zinazotumika katika kuwashia moto. Lakini tafsiri halisi ya “kibiriti” au “kiberiti” sio hiyo. Kibiriti ni aina ya mawe, yanayopatikana duniani, yajulikanayo kwa jina hilo la kibiriti au Salfa..Kwa lugha ya kiingereza ni “Sulfur”.

Mawe haya kwa mwonekano yana rangi ya “manjano iliyofifia”..Tabia ya mawe haya ni kwamba yanawaka “kiwepesi” kama vile mafuta ya taa yanavyowaka kiwepesi yanapokutana na moto.. kadhalika na mawe haya ni myepesi kuwaka yanapokutana na moto.

Katika hali yake ya asili yanapokutana na moto kidogo tu! Yanaanza kuyeyuka taratibu taratibu na mwisho kuwa Uji mzito mweusi, kama tope!..ambao ni wa moto sana, usiozimika kirahisi, mfano wa Magma ya volkano. Lakini pia jiwe hilo hilo, likipelekwa kiwandani linaweza kuchanganywa na malighafi nyingine kutengeneza bidhaa nyingine zinazowaka kirahisi kama “Njiti za kiberiti” au “Unga wa risasi”. Lakini katika hali yake ya asili jiwe hilo la Salfa(kiberiti) likichomwa bila kuchanganywa na kitu kingine chochote, linayeyuka na kuwa tope zito la moto.(Tazama video chini, mwisho wa somo)www.wingulamashahidi.org

Lakini tukirudi kwenye biblia tunaona sehemu kadhaa jiwe hili la Salfa(kiberiti) likitajwa.

Sehemu ya kwanza lilitajwa kipindi cha Sodoma na Gomora, wakati Bwana alipoiangamiza miji ile kwa moto. Biblia inasema moto na kibiriti vilishuka kutoka mbinguni.

Luka 17:28 “Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga;

29 lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma KULINYESHA MOTO NA KIBIRITI kutoka mbinguni vikawaangamiza wote”.

Kiberiti kinachozungumziwa hapo ni hayo mawe ya Salfa yaliyochanganyikana na moto, ambayo yalishuka kutoka juu..Na yaliposhuka moja kwa moja yakaanza kuyeyuka na kuwa TOPE ZITO JEUSI kama la volcano na kuchoma kila kitu.

Mpaka hapo utakuwa umeshaanza kuelewa kwanini Jehanamu ya moto, sehemu nyingine inafahamika kama ZIWA LA MOTO. Kwasababu huwezi kutaja neno ziwa bila kumaanisha “kimiminika” hivyo ziwa la moto maana yake ni “ni moto mwingi ulio katika mfumo wa kimiminika” mfano wa huo moto wa KIBIRITI (Salfa).

Ufunuo 21:7 “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ZIWA LIWAKALO MOTO NA KIBERITI. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Utasoma tena neno hilo katika..

Ufunuo 14:9 “Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake,

10 yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; NAYE ATATESWA KWA MOTO NA KIBERITI mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo.

Na pia Ufunuo 19:30 inazungumzia jambo hilo hilo…

Ufunuo 19:20 “Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ZIWA LA MOTO LIWAKALO KWA KIBERITI;

Na mwisho neno hilo limetajwa katika…

Ufunuo 20:10 “Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, AKATUPWA KATIKA ZIWA LA MOTO NA KIBERITI, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele”.

Sasa kwanini biblia imesema shetani na malaika zake WATATESWA katika Moto na Kiberiti, na SI WATACHOMWA TU!!.

Ni kwasababu Moto wa kiberiti ni tofauti na moto wa kawaida, moto wa kawaida wenyewe unaunguza tu! Na kuteketeza, lakini moto ulio katika mfumo wa kimiminika, tena kama uji uji huo ni unatesa.. Ndio maana kuungua kwa moto wa kawaida ni heri kuliko kuungua kwa vimiminika kama maji au uji..

Wanaofanya kazi za kuyeyusha Salfa(kibiriti) wanakuwa katika uangalifu mkubwa sana kwasababu wanasema moto ule ni mbaya kuliko moto mwingine wowote kwasababu “ule uji wake unapogusa mwili unakuwa unagandamana na ngozi” kwahiyo ili kuuondoa ni lazima ngozi ichubuke, na unakuwa na maumivu makali sana yanayotesa. Ndicho kilichowatokea watu wa Sodoma na Gomora, (walikufa kwa mateso na si kwa kuchomeka tu basi!.)

Na ndicho kitakachowakuta watu wote watakaotupwa katika lile ziwa la Moto.. watateswa katika ziwa la moto.

Swali ni je!, umempokea Yesu?.. Maandiko yanasema.. “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ZIWA LIWAKALO MOTO NA KIBERITI.”

Je na wewe ni miongoni mwa wachukizao?, ni miongoni mwa wachawi, ni miongoni mwa wazinzi na waabudu sanamu?. Kama ndio!, basi tubu leo kwasababu Neema ya Kristo bado ipo, Ziwa la moto kaandaliwa shetani na malaika zake lakini si sisi!, lakini endapo tukiasi kama shetani alivyoasi basi na sisi tutaadhibiwa vile vile kama wao katika ziwa la moto.

Huko ni sehemu ya Mateso, moto ule ni kwa lengo la kutesa, na sio kuchoma tu!.

Bwana atusaidie tusifike huko, bali tuishi maisha ya kumpendeza yeye na kuyaishi maagizo yake.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Whatsapp: +255693036618
 
Top